Jumanne, 6 Mei 2014

JESHI LA POLISI LAJIPANGA KUKOMESHA UKATILI NA UNYANYASAJI WA WATOTO.


Na Demetrius Njimbwi - Jeshi la Polisi

Mkuu wa Dawati la Jinsia Nchini Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Adolfina Chialo, amewataka askari wote nchini hususan wale waliopo katika dawati la jinsia kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi ili kukomesha vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto. 

Hayo ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa semina ya mafunzo ya siku tano yanayotolewa kwa Maafisa na askari wa Jeshi la Polisi katika mkoa wa Dar es salaam, ambapo washiriki hao watapatiwa mafunzo ya namna ya kukabiliana na makosa ya ukatili wa kijinsia. 

Kamishna Chialo, alisema kuwa, ili kutokomeza makosa yatokanayo na ukatili wa kijinsia na unyanyasaji kwa watoto, ameihasa jamii kutofumbia macho uovu au aina yeyote ya ukatili na badala yake kuripoti jambo hilo mahala husika au  katika madawati ya jinsia ya Polisi katika kituo chochote cha Polisi  ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa ambapo kwa sasa jumla ya madawati ya jinsia 417 yameanzishwa hapa nchini. 

Kwa upande wake mgeni rasmi wa semina hiyo ambaye pia ni Afisa Ustawi wa Jamii, Bi. Eva Mbilinyi, alisema Kuwa, lengo kuu la mafunzo haya ni kuwasaidia askari Polisi kwa kuwajengea uwezo katika utendaji wao wa kazi na namna sahihi ya kuwahudumia waathirika wa ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa watoto. 

Bi. Eva Mbilinyi, aliongeza kuwa, bila ulinzi, malezi na makuzi sahihi kwa watoto ni wazi kuwa, taifa haliwezi kupiga hatua katika maendeleo hivyo jamii inatakiwa kuhakikisha kuwa, inamlinda mtoto dhidi ya ukatili wa aina zote za unyanyasaji alisema.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni