Jumanne, 29 Aprili 2014

HALMASHAURI NA WADAU WA JIJI LA MWANZA WAANZA MAANDALIZI YA SHEREHE ZA KUADHIMISHA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA JUNI 16.

Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi inayoundwa na wadau wa watoto jijini Mwanza Bw. Godfrey Salumu akifafanua utaratibu mzima wa utendaji kazi wa kamati ndogo ndogo zilizoundwa kwa wajumbe (hawapo pichani) ili kuweza kufanikisha maadhimisho hayo.

Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya jiji la Mwanza Bi Eluminata Mwita akisikiliza jambo kwa makini toka kwa wajumbe (hawapo pichani). 

Mkurugenzi wa Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Wasichana, KIVULINI Bw Ramadhani Masele (kushoto) ambae pia ni mjumbe wa kamati ya ndogo ya Uratibu, Mipango na Fedha akiteta jambo na mjumbe mwenzake wakati wa kikao hicho.

Wajumbe wa Kikao cha kwanza cha maandalizi ya Sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika itakayofanyika Juni 16 chini ya kauli mbiu ya “Kuondoa Mila Zenye Kuleta Madhara kwa Watoto ni Jukumu Letu Sote”. 

Uongozi wa kamati ya maandalizi ya sherehe ya siku ya Mtoto wa Afrika wilaya ya Nyamagana, Mwanza. Kulia ni Bw Godfrey Salumu ambae ni Mwenyekiti wa kamati, Bw. Devis Mrope (katikati) ambae na Katibu, kushoto ni Katibu Msaidizi Bi. Francisca Michael.

Halmashauri pamoja na wadau toka mashirika na taasisi za kutetea na kulinda haki za watoto jijini Mwanza wameanza rasmi vikao vya maandalizi ya kuadhimisha sherehe za siku ya mtoto wa Afrika inayoadhimishwa kila Mwaka Juni 16.

Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri wa Jiji la Mwanza chini ya Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri hiyo Bi. Eluminatha Mwita wajumbe walikubaliana kuadhimisha siku hiyo katika Kata ya Buhongwa, kwa Wilaya ya Nyamagana.

Siku ya mtoto wa Afrika huadhimishwa kimataifa kote duniani kwa lengo la kutambua thamani, utu, na umuhimu wa mtoto duniani. Maadhimisho haya hufanywa kila juni 16 tangu ilipotangazwa kuwa siku rasmi mwaka 1991 na jumuiya ya umoja wa Afrika.

Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho Afisa Maendeleo Jamii wa Jiji la Mwanza Bi. Eluminatha Mwita alisema kuwa kauli Mbiu ya mwaka huu ni “Kuondoa Mila Zenye Kuleta Madhara kwa Watoto ni Jukumu Letu Sote” na kufafanua kuwa kauli hiyo inalenga kuwasisitiza wazazi na walezi kuacha mila potofu zenye kuleta madhara kwa watoto.

Bi Eluminatha alisema kuwa “Kauli mbiu hiyo ina lenga kuangalia mila zote kandamizi na potofu zinazotokana na jamii husika katika malezi ya mtoto na kusababisha madhara mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa watoto wa mitaani, kubakwa kwa watoto, kukosa elimu, afya na malezi bora pamoja na vifo kwa watoto hawa”.

Kikao hicho cha kwanza kiliweza kuchagua viongozi wa kamati hiyo ya maandalizi, mwenyekiti aliyechaguliwa ni Godfrey Salum huku katibu ni Devis Mrope na katibu msaidizi akichaguliwa Francisca Michael, baada ya kupata viongozi kamati nne ziliundwa na wajumbe, Kamati ya Uratibu, Mipango na Fedha, Kamati ya Usafiri na Ulinzi, Kamati ya Mapambo na Burudani pamoja na kamati ya Hotuba na Habari.

Imeandaliwa na Afisa Habari wa Kamati ya Maandalizi
Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika - Mwanza
Hassan Mrope

0713441892

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni