![]() |
Baadhi ya Washirka wa Maisha Plus 2014 wakitoa mawazo yao katika semina hiyo |
![]() |
Washiriki wa Maisha Plus 2014 wakipewa vijitabu vinavyohusu sheria mbalimbali |
![]() |
Washiriki wa Maisha Plus wakifuatilia maelezo toka kwa wanasheria (hawapo pichani) |
![]() |
Moja ya kundi toka kwa washiriki wa Maisha Plus wakifanya mjadala |
![]() |
Mwanasheria toka shirika la Msaada wa Kisheria kwa Wanawake, WLAC |
Ikiwa ni siku ya tatu toka Mama Shujaa wa chakula waingie kijijini
Maisha Plus na siku ya 37 toka mashindano hayo yaanze rasmi, jopo la
Wanasheria kutoka shirika lisilo la kiserikali la WLAC juzi lilitua
kijijini hapo kwa ajili ya kutoa mafunzo mbalimbali ya kisheria kwa
wanakijiji hao.
Wanasheria hao ambao ni Faudhia Yasin, Sarah
Mambea na Juvenile Rwegasira walianza kwa kuwagawa washiriki katika
makundi matatu na kisha kuwataka wajadili visa walivyopewa.
Visa
hivi vitatu vililenga kupata ufahamu wa wanakijiji juu ya mambo
yanayohusiana na Mjane na urithi, sheria ya ndoa na talaka pamoja na
ukatili dhidi ya wanawake.
Makundi yawasilisha visa
Kundi
la kwanza liliwakilishwa na washiriki Mbonimpaye Nkoronko kutoka
Mtwara, Boniphace Meng’anyi kutoka Dar es salaam na Ngabonziza Daniel
kutoka nchini Rwanda. Vijana hawa katika kisa chao waligundua kwamba mtu
akishakuwa katika ndoa kwa muda wa miaka mitatu tayari anakua mwanandoa
halali.
Kundi hili lilitoa mapendekezo ya kutolewa kwa elimu
juu ya masuala ya ndoa kabla ya watu kuingia katika ndoa na uwepo wa
sheria za kuondoa ukatili na kuleta usawa katika jamii zetu. Boniphace
alisisitiza kwamba uwepo wa sheria madhubuti ndio mkombozi pekee wa
wanyonge kwani bila hivyo watu walio matajiri wanapendelewa.
Mshiriki Ally Thabit kutoka Mwanza alichaguliwa kutoa mrejesho wa kundi
namba mbili ambao kisa mkasa chao kilimuhusu Bwana Musa ambaye alifungua
akaunti tatu za siri na pia kujenga hoteli kisiri bila mkewe kufahamu,
kisa hicho mwishoni kinaonyesha Bwana Musa alifariki ghafla na hivyo
kuleta msuguano mkali sana katika familia yake kuhusu mgawanyo wa mali.
Huku akijibu maswali ya mirathi yaliyojitokeza katika kisa hicho Ally
anataja, miongoni mwa hasara nyingine, kwamba kwanza haki ya urithi
imepotea, pili usiri wa baba umekuwa kikwazo katika familia kupata haki
ya msingi lakini tatu kwamba huenda wakati Bwana Musa anafariki kulikuwa
na pesa nyingi katika akaunti yake benki ambazo zingeisaidia familia
yake ambayo kwa mujibu wa kisa hicho hivi sasa familia hiyo inakumbwa na
janga kali la umaskini.
Katika kuelezea umuhimu wa wosia; Ally
aliendelea kusema kwamba wosia huondoa utata inapotokea kifo na vilevile
wosia huondoa chuki na fitna baina ya ndugu na jamaa.
Mwanamke anaweza kuwa msimamizi wa mirathi
Naye Faudhia Yassin ambaye ni mratibu wa kampeni ya TUNAWEZA kutoka
WLAC aliwaeleza wanakijiji kwamba Mwanamke amekuwa akitengwa sana katika
ugawaji mali hivyo ni muhimu jamii kutambua kwamba hata wanawake
waliofiwa na waume zao wanaweza kuwa wasimamizi halali wa mirathi.
Faudhia alisema ikitokea baba amefariki, familia ichukue cheti cha kifo
na kukipeleka mahakamani kuomba mahakama imuidhinishe waliyempendekeza
kuwa msimamizi wa mirathi.
Ndoa halali ni ipi?
Kundi la
tatu liliwakilishwa na Mama Shujaa wa chakula Grace G.D. Mahumbuka
kutoka Kagera pamoja na vijana wa Maisha Plus ambao ni Bakari Khalid
kutoka Shinyanga na Said Kawawa kutoka nchini Uganda.
Kundi hili
liligundua kwamba mtoto wa kike hathaminiki kama ilivyo kwa mtoto wa
kiume, lakini elimu pia ya uelewa juu ya mambo ya haki ni duni. Sehemu
ya kisa hicho iliwataja watu wawili wa jinsia tofauti walioishi pamoja
kwa kipindi cha miaka 12 bila kuwa na ndoa hata ya kimila.
Aidha
kundi hili lilipendekeza sheria ya ndoa ya Tanzania iboreshwe na kwamba
ifahamike kuwa mtoto wa kike ana haki ya kurithi sehemu ya mali ya
wazazi wake sawa sawa na ilivyo kwa mtoto wa kiume.
Waliendelea
kwa kushauri kwamba inapotokea tatizo katika ngazi ya familia baina ya
mke na mme basi aliyetendewa ukatili ajaribu kusuruhisha katika ngazi ya
familia ikishindana basi aende katika ustawi wa jamii, baraza la kata,
ofisi za ushauri wa kisheria za mashirika ya kiserikali na yasiyo ya
kiserikali kama itashindikana kote huko basi mwisho achukue hatua za
kisheria za kimahakama.
Akifafanua kuhusu hoja hii, Mwanasheria
Juvenile Rwegasira kutoka WLAC alisema kwamba watu wawili wa jinsia
tofauti wakiishi pamoja kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo na jamii
ikafahamu kwamba hawa ni mme na mke, hiyo kisheria inaitwa dhana ya
ndoa.
Mwanasheria Rwegasira alisisitiza kwamba ni lazima iwe
miaka miwili mfululizo na sio ile ya kuja miezi miwili na kuondoka na
kuja tena na kuondoka.
Hata hivyo, Bw. Rwegasira alitoa angalizo
kwamba ndoa hii ni rahisi sana kukanushika hivyo akasisitiza umuhimu wa
kuhitaji tamko la Mahakama kuidhinisha dhana ya ndoa.
Akiendelea Bw. Rwegasira alisema kwamba ndoa hii ni ya kienyeji mno na
haina cheti hivyo ikitokea mmoja amefariki inaleta shida sana kwenye
ugawaji wa mali.
Pata msaada wa kisheria BURE
WLAC ni
kituo cha msaada wa kisheria kwa wanawake. Kwa wenye matatizo ya
Mirathi, Ndoa, Ardhi, Elimu, Ajira, Matunzo ya Watoto na Mengineyo
wapige simu BURE kwenda namba 0800780100
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni