Ilikuwa
ni saa moja na nusu jioni siku ya
jumapili wakati, Anaheri (siyo jina lake
halisi) alipokuwa akitoka dukani alikotumwa na mama yake. Si yeye wala mama
yake waliokuwa na wasiwasi wowote, kwani mara kadhaa amekuwa akitumwa nyakati
hizo.
Lakini
kama balaa linavyoweza kushtukiza, siku hiyo Anaheri, alikamatwa na wanaume
wawili waliokuwa wamejificha kichakani. Wakamziba mdomo na kumwingilia. Hawakuishia
hapo, waliamua kumvunja shingo na kumuua
binti huyo mwenye miaka 11 tu.
Hii
ndiyo hali halisi nchini, ubakaji na ulawiti vimeshika kasi kiasi cha kutishia
amani, utulivu na uhuru.
Takwimu
za Kitaifa za makosa ya unyanyasaji wa kijinsia kwa mwaka 2012 zinaonyesha
wanawake 5745 walibakwa kwa mwaka. Kati
yao wanawake wenye umri wa miaka 19 na kuendelea walikuwa 5389 na watoto wenye
umri wa chini ya miaka 18 walikuwa 356.
Makosa
hayo hayakuishia hapo kwani wanaume na wanawake pia waliendelea kulawitiwa, kwa
mwaka 2012 pekee wanaume 691
walilawitiwa. Kati yao, wanaume
waliolawitiwa wenye umri wa zaidi ya miaka 18 ni 456 na watoto ni 235.
Wanawake
pia hawakuachwa kwani kwa mwaka huo
huo, wanawake 35 walilawitiwa ambao walikuwa na umri wa miaka 19 na
kuendelea wakati watoto waliolawitiwa walikuwa ni 11.
Vilevile
mauaji ya vikongwe yaliendelea kwa kasi kubwa, kwa mwaka 2012, vikongwe 629
waliuawa. Kati ya hao, wanawake walikuwa
402 na wanaume 227.
Waziri
wa Maendeleo ya Jamii, Jnsia na Watoto, Sophia
Simba anasema kazi kubwa ambayo wizara ilifanya ni kuunda sheria kali
kuwaadhibu wabakaji na walawiti.
“Kwa
jambo hili la kuunda sheria nafikiri tumefanikiwa kwa sababu adhabu ya miaka 30
si ndogo, lakini tunahitaji wanajamii washiriki kuzuia ubakaji,” anasema.
Waziri
Simba pia anawataka waandishi wa habari kufanya kazi ya ziada ili kuripoti
kuhusu ubakaji kwa kuandika, kufanya utafiti na kuhamasisha.
Naibu
Kamishna Mkuu wa Polisi, Adolphina Chialo anasema unyanyasaji bado ni tishio kwa
Watanzania licha ya juhudi kufanyika
kila siku kuwachukulia hatua wanaofanya uhalifu huo.
Chialo
anasema matukio ambayo huripotiwa ndiyo
yaliyowekwa kwenye takwimu, hivyo kuna uwezekano kuwa yapo matukio ambayo
hayaripotiwi.
“Zamani
kesi kama hizi zilikuwa zinaripotiwa chumba cha mashtaka polisi, lakini
tuliamua kuanzisha Dawati la Jinsia kwa ajili ya usiri wake. Dawati hili
linapokea malalamiko kutoka kwa wanaume, wanawake na watoto. Tunaposema jinsia hatumaanishi ni
wanawake pekee,” anasema
Anasema unyanyasaji wa aina zote upo na
kuongeza kuwa hapo zamani wanawake pekee ndiyo walioonekana kunyanyasika lakini
hivi sasa, hata wanaume wananyanyasika.
Kwa
mfano, wapo wanaume ambao wananyanyaswa na wake zao lakini si kwa kupigwa au
kubakwa bali matusi na kunyimwa baadhi ya huduma hasa kipato kinaposhuka.
“Wanaume
wanafika hapa, wanaeleza manyanyaso yao
wanayoyapata kutoka kwa wake zao na hatua zinachukuliwa. Kwa mfano mawasiliano,
kupikiwa, ” anasema.
Anasema suala kubwa zaidi ni ubakaji na vipigo
ambapo vipigo vinahusisha watoto kuchomwa moto na kutukanwa.
“Sasa
hivi haya matukio yanaonekana kuwa mengi kwa sababu yanaripotiwa. Zamani watu walikuwa wanayaficha au wanadhani hakuna
pa kuripoti lakini sasa hivi wamejua kuwa kuna suluhisho,” anasema.
Anasema mikoa ambayo ilidhaniwa kuwa ingekuwa
na matukio mengi ya ubakaji, kama Mwanza na Kagera haina matukio mengi kwa
sababu ya mila zinazowazunguka.
Kwa mfano, Wilaya ya Kinondoni, mikoa ya Mbeya
na Morogoro ilikuwa na matukio mengi zaidi ya ubakaji kuliko Kagera,
Mwanza au Tarime jambo ambalo Kamishna Chialo anasema linasababishwa na mila.
Kinondoni ina matukio 414 ya ubakaji.
“Kwa
mfano Mwanza, kuna hii mila ya Chagulaga, kwao mwanamke hawezi kuripoti kwa
sababu kwao ni sehemu ya mila. Lakini kwa sababu ya elimu baadhi ya mikoa
imeamka na wanaripoti,” anasema.
Anasema
unyanyasaji wa kipigo na mashambulizi pia hauripotiwi kwenye baadhi ya maeneo
kwa sababu ya mila. Kwa baadhi ya mila ni haki na sheria kwa mwanamke kupigwa
na mume wake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni