Jumanne, 1 Aprili 2014

WANAFUNZI WA KIKE WANAVYOANGUKIA KWENYE MIKONO YA WANAUME WAKWARE


Mwanafunzi wa kike akidanganywa jambo na mtoto wa kiume, hali hii huchangia zaidi kupotea kwa ndoto za wanafunzi wa kike. Picha na na habari: Mwananchi 
Picha hii inatoa ushuhuda wa vikwazo wanavyokumbana navyo wanafunzi wa kike wakiwa njiani kwenda au kurudi shule.
Mwandishi wetu alimwona mwanafunzi huyu akizongwa na kijana huyu mkware katika eneo la makaburi ya Bahi Road mkoani Dodoma.
Japo wahusika walionekana kujuana, msichana huyu anayesoma Shule ya Sekondari Kikuyu iliyopo Manispaa ya Dodoma, alikiri kuwa maongezi yao yalikuwa yakielekea kubaya kiasi cha kuamua kukimbia.
Kadhia hii ilimkumba msichana huyu akiwa njiani. Anapoishi na ilipo shule kuna umbali wa karibu kilomita tano.
Vikwazo kwa watoto wa kike
Pamoja na mikakati iliyopo ya kuwasaidia watoto wa kike kupata elimu, hali halisi katika maeneo mengi nchini inaonyesha kuwa bado kuna vikwazo mbalimbali vinavyowazuia wasichana kupata haki hiyo ya msingi.
Kwa mfano, mara kwa mara wadau wa elimu kupitia ripoti zao wamekuwa wakisema watoto wa kike nchini wakiwamo wanafunzi hawako salama.
Wanafunzi hao ni waathirika wakubwa wa vitendo mbalimbali vya unyanyasaji wa kijinsia ikiwamo kubakwa. Ukweli ni kwamba wanafunzi wa kike hawako salama nyumbani, njiani wanapoelekea au kurudi shule na hata shuleni kwenyewe.
Unyanyasaji njiani ni kwa sababu shule nyingi hasa zilizo maeneo ya vijijini, ziko mbali na makazi ya watu, hivyo wasichana wanalazimika kutembea masafa marefu.
Umbali huu una athari kwa watoto wa kike, kama vile kuchokozwa na wahuni, kurubuniwa na wanaume wakware na hata kubakwa.
Katika baadhi ya maeneo, wanafunzi hao wanalazimika kupita katika maeneo hatarishi kama vile porini. Tukio la mwanafunzi huyu ni ushahidi kuwa wasichana hawako salama. Hata baadhi ya matukio ya ujauzito shuleni huanza kwa namna hii.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni