Maafisa Miradi pamoja na Maafisa
Wakaguzi na Tathmini Miradi toka mashirika matano ya Kiraia yanayopata ruzuku
kutoka Mfuko wa Msaada wa Kisheria (LSF) Tanzania, yamemaliza ziara ya
kimafunzo ya siku tatu katika Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na wasichana
Tanzania, KIVULINI la jijini Mwanza, ziara iliyolenga kujifunza na kuboresha
ufanyaji kazi wa mashirika hayo kupitia Miradi mbalimbali inayoendeshwa na
KIVULINI.
Mashirika hayo matano toka mikoa ya
Kagera, Shinyanga, Mara, na Tabora yalianza mafunzo hayo Jumatatu ya tarehe 28
Aprili, 2014 na kumaliza mafunzo hayo tarehe 30 Aprili, 2014 kwa kutembelea
Wasaidizi wa Kisheria wanaofanya kazi ya kutoa elimu na ushauri wa kisheria
katika vijiji mbalimbali vya Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba chini ya shirika
la KIVULINI kupitia mradi wa Msaada wa Kisheria unaofadhiliwa na LSF.
Akizungumza mara baada ya kumalizika
kwa Ziara hiyo Mkurugenzi wa Shirika la KIVULINI Bw. Ramadhan Masele
aliwashukuru maafisa wote toka mikoa hiyo mitano ya kanda ya ziwa kwa kuhudhuria
mafunzo hayo lakini pia aliwashukuru Mfuko wa Msaada wa Kisheria kwa heshima
waliyowapa KIVULINI kuwa kituo cha mafunzo kwa asasi nyengine.
“Ziara hii imetoa hamasa nzuri hasa
kwa upande wa kimahusiano baina ya Asasi zinazotekeleza mradi wa msaada wa kisheria
kwa kanda ya ziwa, pia uzoefu tuliobadilishana kwa siku zote tatu za mafunzo
naamini utaenda kuimarisha utendaji kazi wa asasi zetu na kuinua hali ya maisha
ya Watanzania kupitia sisi” alisema Mkurugenzi wa KIVULINI Bw Ramadhan Masele.
“Lakini pia tuwashukuru wadau wetu
wakubwa katika mradii huu wa msaada wa kisheria, LSF, kwa ubunifu waliouleta wa
kutuwezesha kukutana pamoja na kubadilishana uzoefu katika utendaji kazi, na
hivyo hivyo shukrani zetu ziende kwa Foundation for Civil Society kwa kushirkiana
na SLF kuwa pamoja nasi, tunaomba huu uwe ni mwanzo tu na usiwe mwisho”
alimalizia Bw Masele
Ziara hiyo imeratibiwa na LSF kwa
kushirikiana na Foundation For Civil Society kutoa hamasa na kuinua utendaji
kazi wa Asasi za Kiraia nchini katika kuhakikisha asasi hizo zinatoa matokeo
bora katika mradi wa Msaada wa kisheria.
Mashirika yaliyohudhuria ziara hiyo
ya Kimafunzo ni Jamii Salama Development Volunteers (JSDV) toka Tabora, Centre
for Widows and Children Assistance (CWCA) la mkoani Mara, Mama’s Hope
Organization for Legal Aid (MHOLA), Paralegal Aid Centre Shinyanga (PACESHI),
Sheria na Haki za Binadamu (SHEHABITA) la mkoani Mara.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni