Na Hawra Shamte,Mwananchi
Kwanza niwape pongezi
wanawake wote duniani kwa kuadhimisha siku yao.
Pili napenda nitumie
nafasi hii kuangalia hali ya wanawake tabaan katika maeneo mbalimbali duniani.
Wanawake wanapewa
kipaumbele katika mipango ya maendeleo katika nchi nyingi kwa sababu moja kuu;
kwa kuwa wao ndiyo waathirika wakuu wa madhila, vita na kila balaa linalotokea
duniani.
Tuangalie wanawake
wanaotaabika katika maeneo yenye migogoro kama vile Syria na Jamhuri ya Afrika
ya Kati. Wanawake ndiyo wanaohangaika na watoto, ndiyo wanaoathirika na vitendo
vya ubakaji na unyanyasaji mwingine wa kijinsia.
Wanawake ndiyo
wanaochukua jukumu la kuhudumia familia takriban kwa nyakati zote. Wakati
mwanamume anaweza kujibaraguza kama nyumbani hakuna chakula, mwanamke
atagangamala kuhakikisha chakula kinapatikana kwa ajili ya watoto wake. Atauza
vitumbua/maandazi, atatembeza ndizi na mihogo mibichi mitaani, atakopesha
khanga, viatu na madira, atalima na atatumika nyumbani kwa watu ili angalau
apate vijisenti kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya familia yake.
Kimaumbile mwanamke ni
mtu wa amani na utulivu, katika mazingara ya fujo, ugomvi na vita. Utu wa
mwanamke huwa uko shakani, hana uhakika wa mustakabali wa maisha ya familia
yake. Mwanamke kama mwamvuli, yuko radhi yeye aloe kwa kuihifadhi familia yake.
Wakati wanaume wako
‘bize’ kupigania madaraka, wanawake wameshughulika kulea/kukuza vijana wao.
Wangependa watoto wao wawe na maisha bora, watoto wao wapate elimu yenye
manufaa, watoto wao wawe na afya njema, watoto wao wale, wacheze, wakue na
waishi wakiwa na furaha.
Mutribu mmoja alielezea
maisha ya mshumaa akasema kuwa ‘unawaka na kuteketea, kufurahisha umati,’ hali
hiyo kwa kiasi kikubwa inaakisi tabia ya mwanamke, kila mara hufikiria furaha
ya wengine kabla ya kufikiria furaha yake.
Ni kwa mintarafu hiyo,
ndiyo yakawepo maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, kwa sababu angalau
dunia ipate nafasi ya kutafakari umuhimu, masilahi na fursa za kiumbe huyu
aliye na sifa lukuki lakini wenye nguvu hawampi fursa ya kuonyesha vipaji
vyake.
Fursa anazonyimwa
mwanamke ni nyingi na zinatofautiana kutoka jamii moja hadi nyingine. Zipo
jamii zinazomnyima mwanamke fursa ya kupata elimu, zipo zinazomnyima fursa ya
kufanya kazi, wapo wasiompa mwanamke nafasi ya kuongoza, wapo pia wanaomwona
mwanamke kama kitu cha kuwastarehesha na kuwatimizia mshawasha wao wa matamanio
ya mwili na kisha kumdharau kwa kumtupa kama ‘karatasi ya chooni.’
Sheria, imani za kidini
na hata mila na desturi nyingi duniani huthamini zaidi wanaume kuliko wanawake.
Ziko jamii ambazo ilikuwa akizaliwa mtoto wa kike ndani ya nyumba huchukuliwa
na kuzikwa akiwa angali hai. Ziko jamii ambazo ilikuwa mume akifariki dunia,
huzikwa pamoja na mke wake aliye hai.
Ziko jamii ambazo hadi
leo baba na mama wakitambua tu kuwa mtoto aliyeko tumboni ni wa kike, huhiari
kuitoa mimba kabla haijazaliwa.
Ilimradi orodha ya
madhila na manyanyaso kwa wanawake ni mengi. Lakini pamoja na matatizo hayo
yote ya kijamii, ya kisiasa na hata ya kiitikadi, je, mwanamke mwenyewe
anajitambua? Hapo ndipo tunapopaswa kupang’ang’ania.
Mwanamke anapaswa
atambue utu wake na nafasi yake katika jamii, kwamba yeye ni binadamu sawa na
mwanamume na mwenye haki sawa na mwanamume kimazingira/kijamii na siyo
kimaumbile. Hivyo mwanamke anapaswa ahakikishe anaipata nafasi hiyo katika
jamii yake.
Wakati pale mwanamume
haki zake anapozikuta kwenye sahani ya fedha, mwanamke analazimika azipiganie,
ndiyo maana zinatokea dhana za ushirikishwaji na uwezeshwaji kwa sababu kwa
kiasi kikubwa hatamu za dola na mamlaka zimeshikwa na wanaume.
Kwa karne tatu sasa,
wanawake wamekuwa wakipigania haki zao na nafasi zao katika jamii, toka karne
ya 19, mwaka 1908 wakati wafanyakazi wanawake wa nchini Marekani walipoandamana
kupinga uonevu waliokuwa wakifanyiwa na waajiri wao, lakini mpaka leo
unyanyasaji wa wanawake bado ni tatizo kubwa katika jamii nyingi.
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa, Koffi Annan aliwahi kusema: “Ukatili dhidi ya wanawake
unasababisha simanzi isiyoelezeka, huumiza familia kutoka kizazi kimoja hadi
kingine na kushusha kiwango cha maisha ya familia. Ukatili huo husababisha
wanawake washindwe kufikia viwango vya juu vya utendaji wao, unadhibiti ukuaji
wa uchumi na kudumaza maendeleo.”
Kaulimbiu ya mwaka huu
ni ‘Chochea mabadiliko, kuleta usawa wa kijinsia,’ bila shaka mabadiliko haya
yanapaswa kuchochewa kuanzia ngazi ya familia, jamii hadi taifa na anayepaswa
kuchochea mabadiliko haya ni mimi na wewe.
Iliniduwaza kidogo wiki
iliyopita wakati wa mjadala wa kanuni za Bunge Maalumu la Katiba, wakati
walipokuwa wakijadili nafasi za uongozi katika Bunge hilo kwa mtazamo wa
kijinsia.
Tuliona jinsi wanaume
walivyokuja juu lilipokuja wazo, ikiwa Mwenyekiti atakuwa mwanamume, Makamu
Mwenyekiti awe mwanamke, kusema kweli walilipinga wazo hilo kwa hoja za ajabu
kabisa.
Waliolitoa wazo lile
hawakukusudia kutaka upendeleo, bali walitaka hali ya usawa wa kijinsia
izingatiwe katika kuongoza Bunge hilo Maalumu na uzingatifu huo usiwe kwa
misingi ya upendeleo wa wanawake tu, bali fursa wapewe wanawake wenye uwezo wa
kuongoza.
Hali ile
ilitudhihirishia kuwa tutaendelea kupiga kelele za jinsia kwa muda mrefu na
pengine kwa karne nyingi zaidi kabla hatujafikia hatua maridhawa, hatua ya
kumwona mwanamke kama kiumbe mwenye uwezo sawa na mara nyingine mkubwa zaidi ya
mwanamume na kumpa nafasi ya kuonyesha uwezo wake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni