Jumapili, 11 Mei 2014
Jumanne, 6 Mei 2014
JESHI LA POLISI LAJIPANGA KUKOMESHA UKATILI NA UNYANYASAJI WA WATOTO.
Na Demetrius Njimbwi - Jeshi la Polisi
Mkuu wa Dawati la Jinsia Nchini Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Adolfina Chialo, amewataka askari wote nchini hususan wale waliopo katika dawati la jinsia kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi ili kukomesha vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.
Hayo ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa semina ya mafunzo ya siku tano yanayotolewa kwa Maafisa na askari wa Jeshi la Polisi katika mkoa wa Dar es salaam, ambapo washiriki hao watapatiwa mafunzo ya namna ya kukabiliana na makosa ya ukatili wa kijinsia.
Kamishna Chialo, alisema kuwa, ili kutokomeza makosa yatokanayo na ukatili wa kijinsia na unyanyasaji kwa watoto, ameihasa jamii kutofumbia macho uovu au aina yeyote ya ukatili na badala yake kuripoti jambo hilo mahala husika au katika madawati ya jinsia ya Polisi katika kituo chochote cha Polisi ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa ambapo kwa sasa jumla ya madawati ya jinsia 417 yameanzishwa hapa nchini.
Kwa upande wake mgeni rasmi wa semina hiyo ambaye pia ni Afisa Ustawi wa Jamii, Bi. Eva Mbilinyi, alisema Kuwa, lengo kuu la mafunzo haya ni kuwasaidia askari Polisi kwa kuwajengea uwezo katika utendaji wao wa kazi na namna sahihi ya kuwahudumia waathirika wa ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa watoto.
Bi. Eva Mbilinyi, aliongeza kuwa, bila ulinzi, malezi na makuzi sahihi kwa watoto ni wazi kuwa, taifa haliwezi kupiga hatua katika maendeleo hivyo jamii inatakiwa kuhakikisha kuwa, inamlinda mtoto dhidi ya ukatili wa aina zote za unyanyasaji alisema.
Jumatatu, 5 Mei 2014
SHIRIKA LA NELICO NA MABARAZA YA WATOTO WILAYA YA GEITA WAFANYA ZIARA YA KIMAFUNZO KATIKA SHIRIKA LA KIVULINI
Shirika la watoto la New Light Children Center Organization
(NELICO) la mkoani Geita kwa kushirikiana na Idara ya Maendeleo ya jamii Geita,
limeambatana na wawakilishi 20 toka Mabaraza ya watoto ya kata kumi na moja
(11) za wilaya ya Geita kwa ziara ya kimafunzo katika shirika la kutetea Haki
za Wanawake na wasichana, KIVULINI la mkoani Mwanza.
Ziara hiyo ya kimafunzo katika shirika la KIVULINI
imefanyika hapo jana ikiwa na lengo la kujifunza namna KIVULINI ilivyosaidia
Baraza la watoto Mwanza kuweza kuratibu na kutekeleza shughuli zake kikamilifu
na kuwa imara zaidi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mkurugenzi wa NELICO Bi.
Paulina Alex alisema kwamba ziara hiyo imelenga kutoa mafunzo kwa mabaraza ya
watoto wilayani Geita juu ya mbinu za kuratibu na kutekeleza miradi mbalimbali
lakini pia kujua mafanikio na changamoto za shirika la KIVULINI katika kupiga
vita ukatili dhidi ya wanawake na wasichana katika mikoa ya kanda ya ziwa.
“Mabaraza ya watoto ya Geita bado ni machanga sana na
hivyo kufanya safari hii ya mafunzo kuwa ya muhimu sana. Katika safari hii
wawakilishi wa mabaraza ya watoto wameweza kupata elimu kubwa kutoka KIVULINI
na Baraza la watoto la Mwanza (Mwanza Youth and Children Network) ambalo ni zao
la KIVULINI” alisema Bi. Paulina.
Ziara hiyo pia ilikuwa na Bw. Maximillian Kitigwa amabe ni
mwakilishi toka shirika la Plan International ambao ni wadau wakubwa wa watoto
kwa mkoa wa Geita pamoja na Afisa Maendeleo ya jamii wa wilaya ya Geita Bi.
Emma Busanji. Watoto hao pia watafanya ziara katika Mkoa wa Arusha kujionea
juhudi za wadau wa maendeleo katika mkoa huo katika kuwaokoa watoto dhidi
ya kufanyishwa kazi hatarishi hasa katika sekta ya madini.
Kivulini ni shirika lisilo la kiserikali la kutetea na
kulinda Haki za Wanawake na Wasichana. Shirika la Kivulini linahamasisha jamii
(Wanawake, Wanaume na Vijana) kulinda, kutetea Haki za Wanawake na Wasichana
kwa kupinga vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia. Makao makuu ya shirika yapo
jijini Mwanza, Wilaya ya Ilemela, Tanzania.
Ijumaa, 2 Mei 2014
WASICHANA 30 TOKA WILAYA YA ILEMELA NA NYAMAGANA MWANZA WAPATIWA MAFUNZO YA SIKU TANO KUHUSU ELIMU YA UKATILI WA KIJINSIA MAJUMBANI
Mkurugenzi
wa shirika la kutetea Haki za Wanawake na Wasichana KIVULINI lenye makao yake
makuu jijini Mwanza Bw. Ramadhan Masele amefunga rasmi mafunzo ya siku tano yanayolenga
kuwajengea wasichana uwezo wa kutoa
elimu juu ya masuala ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia chini ya mradi wa
kuwashirikisha vijana kuzui Ukatili wa majumbani ikiwa ni pamoja na ukatili wa kingono kwa watoto wa kike na wasichana.
Akizungumza
na washiriki wa mafunzo hayo Bw. Masele aliwataka washiriki wote kutumia elimu
hiyo muhimu waliyoipata kutoa elimu na kuongeza uwelewa zaidi kwa jamii yao
kuanzia ngazi ya familia, marafiki na vikundi mbalimbali na kuwa chachu ya
mabadiliko juu ya kupigania haki za
wanawake na wasichana wanaonyanyaswa kijinsia katika jamii zao.
“Imani
yangu ni kuwa semina hii itakuwa ni kiwanda kizuri cha kuwatengeneza nyinyi
wote kuwa mabalozi wazuri katika jamii, baada ya mafunzo haya tunaamini kuwa
mtakuwa chachu ya mabadiliko katika kutetea na kulinda haki za wanawake na
wasichana kwa kukemea, Kupinga, kuripoti na kuzuia aina zote za ukatili wa
majumbani na kingono kwa wasichana na wanawake na kutoa taarifa pindi vitendo
hivi vinapotokea” alisema Bw. Masele
“Kila
mmoja aliyehudhuria mafunzo haya kwa
nafasi aliyonayo tunaamini anaweza kuwa chachu ya mabadiliko endapo atatimiza
wajibu wake kwenye eneo analoishi. Hili suala la ukatili wa kijinsia si suala
geni nchini hasa eneo hili la kanda ya ziwa hivyo kuna kila sababu ya kuzidisha
mapambano dhidi yake, cha muhimu ni kuzingatia mafunzo mliyopewa na muwezeshaji
wenu” aliongeza Bw. Masele.
Mafunzo
hayo yamefanyika kwa muda wa siku 5 kwa vijana 30 wa kike wenye umri kati ya
miaka 18-24 kutoka wilaya mbili za Nyamagana na Ilemela jijini Mwanza. Lengo la
Mafunzo ni kuwajengea vijana uwezo wao binafsi na uwezo wa kuelimisha jamii hasa
Vijana wenzao kupambana na kupinga
Ukatili dhidi ya wanawake na wasichana katika maeneo wanayoishi.
Mafunzo
yalianza Jumatatu tarehe 28 Aprili, 2014 mpaka tarehe 2 Aprili, 2014 katika
Ukumbi wa Chuo cha Ufundi Stadi, VETA kilichopo Nyakato nje kidogo ya jiji la
Mwanza.
Takwimu
zinaonyesha bado jamii inakabiliwa na ukatili mkubwa wa kijinsia ambapo ubeberu
wa wanaume pamoja na mila na desturi potofu zimeonekana kukandamiza jinsi ya
kike zaidi kuliko jinsi ya kiume, ukatili huo ni wa kijamii, kiuchumi pamoja na
kisaikolojia hivyo kunaitajika juhudi za dhati na makusudi kuweza kukabiliana
na tatizo lilopo kwa jamii.
Akimalizia
mawaidha yake kwa washiriki Bw. Masele alisema lengo la mafunzo hayo ni kuona
mabadiliko katika mfumo juu ya kujali na kuheshimu haki za mwanamke na
wasichana, kwani jamii nyingi zinapambana na mifumo miwili mikubwa, ambayo ni
mfumo dume ambao umekuwa ukiwakandamiza wanawake katika jamii na mfumo wa kitabaka
unaoongeza nafasi kati ya matajiri na masikini.
Shirika
la KIVULINI kwa kushirikiana na Asasi ya Vijana inayojulikana kama Wadada Centre for Solution
Focus Approach ndio waandaji wa mafunzo hayo kupitia mradi wa kuwashirikisha
vijana kuzui Ukatili majumbani na Ukatili wa Kingono chini ya ufadhili wa
Shirika la terre des hommes ch (tdhschweiz) - Fursa kwa Vijana la nchini Switzerland
Kivulini
ni shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na kutetea pamoja na
kulinda Haki za Wanawake na Wasichana. Shiriki la Kivulini linahamasisha jamii
(Wanawake, Wanaume na Vijana ) kulinda, kutetea Haki za Wanawake na Wasichana
kwa kupinga vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia. Makao makuu ya shirika yapo
jijini Mwanza, Wilaya ya Ilemela, Tanzania.
ASASI TANO ZINAZOPATA RUZUKU TOKA MFUKO WA MSAADA WA KISHERIA (LSF) KWA MIKOA YA KANDA YA ZIWA ZAMALIZA ZIARA YA SIKU 3 SHIRIKA LA KIVULINI
Maafisa Miradi pamoja na Maafisa
Wakaguzi na Tathmini Miradi toka mashirika matano ya Kiraia yanayopata ruzuku
kutoka Mfuko wa Msaada wa Kisheria (LSF) Tanzania, yamemaliza ziara ya
kimafunzo ya siku tatu katika Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na wasichana
Tanzania, KIVULINI la jijini Mwanza, ziara iliyolenga kujifunza na kuboresha
ufanyaji kazi wa mashirika hayo kupitia Miradi mbalimbali inayoendeshwa na
KIVULINI.
Mashirika hayo matano toka mikoa ya
Kagera, Shinyanga, Mara, na Tabora yalianza mafunzo hayo Jumatatu ya tarehe 28
Aprili, 2014 na kumaliza mafunzo hayo tarehe 30 Aprili, 2014 kwa kutembelea
Wasaidizi wa Kisheria wanaofanya kazi ya kutoa elimu na ushauri wa kisheria
katika vijiji mbalimbali vya Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba chini ya shirika
la KIVULINI kupitia mradi wa Msaada wa Kisheria unaofadhiliwa na LSF.
Akizungumza mara baada ya kumalizika
kwa Ziara hiyo Mkurugenzi wa Shirika la KIVULINI Bw. Ramadhan Masele
aliwashukuru maafisa wote toka mikoa hiyo mitano ya kanda ya ziwa kwa kuhudhuria
mafunzo hayo lakini pia aliwashukuru Mfuko wa Msaada wa Kisheria kwa heshima
waliyowapa KIVULINI kuwa kituo cha mafunzo kwa asasi nyengine.
“Ziara hii imetoa hamasa nzuri hasa
kwa upande wa kimahusiano baina ya Asasi zinazotekeleza mradi wa msaada wa kisheria
kwa kanda ya ziwa, pia uzoefu tuliobadilishana kwa siku zote tatu za mafunzo
naamini utaenda kuimarisha utendaji kazi wa asasi zetu na kuinua hali ya maisha
ya Watanzania kupitia sisi” alisema Mkurugenzi wa KIVULINI Bw Ramadhan Masele.
“Lakini pia tuwashukuru wadau wetu
wakubwa katika mradii huu wa msaada wa kisheria, LSF, kwa ubunifu waliouleta wa
kutuwezesha kukutana pamoja na kubadilishana uzoefu katika utendaji kazi, na
hivyo hivyo shukrani zetu ziende kwa Foundation for Civil Society kwa kushirkiana
na SLF kuwa pamoja nasi, tunaomba huu uwe ni mwanzo tu na usiwe mwisho”
alimalizia Bw Masele
Ziara hiyo imeratibiwa na LSF kwa
kushirikiana na Foundation For Civil Society kutoa hamasa na kuinua utendaji
kazi wa Asasi za Kiraia nchini katika kuhakikisha asasi hizo zinatoa matokeo
bora katika mradi wa Msaada wa kisheria.
Mashirika yaliyohudhuria ziara hiyo
ya Kimafunzo ni Jamii Salama Development Volunteers (JSDV) toka Tabora, Centre
for Widows and Children Assistance (CWCA) la mkoani Mara, Mama’s Hope
Organization for Legal Aid (MHOLA), Paralegal Aid Centre Shinyanga (PACESHI),
Sheria na Haki za Binadamu (SHEHABITA) la mkoani Mara.
WLAC WATOA MSAADA WA KISHERIA NDANI YA KIJIJI CHA MAISHA PLUS
![]() |
Baadhi ya Washirka wa Maisha Plus 2014 wakitoa mawazo yao katika semina hiyo |
![]() |
Washiriki wa Maisha Plus 2014 wakipewa vijitabu vinavyohusu sheria mbalimbali |
![]() |
Washiriki wa Maisha Plus wakifuatilia maelezo toka kwa wanasheria (hawapo pichani) |
![]() |
Moja ya kundi toka kwa washiriki wa Maisha Plus wakifanya mjadala |
![]() |
Mwanasheria toka shirika la Msaada wa Kisheria kwa Wanawake, WLAC |
Ikiwa ni siku ya tatu toka Mama Shujaa wa chakula waingie kijijini
Maisha Plus na siku ya 37 toka mashindano hayo yaanze rasmi, jopo la
Wanasheria kutoka shirika lisilo la kiserikali la WLAC juzi lilitua
kijijini hapo kwa ajili ya kutoa mafunzo mbalimbali ya kisheria kwa
wanakijiji hao.
Wanasheria hao ambao ni Faudhia Yasin, Sarah
Mambea na Juvenile Rwegasira walianza kwa kuwagawa washiriki katika
makundi matatu na kisha kuwataka wajadili visa walivyopewa.
Visa
hivi vitatu vililenga kupata ufahamu wa wanakijiji juu ya mambo
yanayohusiana na Mjane na urithi, sheria ya ndoa na talaka pamoja na
ukatili dhidi ya wanawake.
Makundi yawasilisha visa
Kundi
la kwanza liliwakilishwa na washiriki Mbonimpaye Nkoronko kutoka
Mtwara, Boniphace Meng’anyi kutoka Dar es salaam na Ngabonziza Daniel
kutoka nchini Rwanda. Vijana hawa katika kisa chao waligundua kwamba mtu
akishakuwa katika ndoa kwa muda wa miaka mitatu tayari anakua mwanandoa
halali.
Kundi hili lilitoa mapendekezo ya kutolewa kwa elimu
juu ya masuala ya ndoa kabla ya watu kuingia katika ndoa na uwepo wa
sheria za kuondoa ukatili na kuleta usawa katika jamii zetu. Boniphace
alisisitiza kwamba uwepo wa sheria madhubuti ndio mkombozi pekee wa
wanyonge kwani bila hivyo watu walio matajiri wanapendelewa.
Mshiriki Ally Thabit kutoka Mwanza alichaguliwa kutoa mrejesho wa kundi
namba mbili ambao kisa mkasa chao kilimuhusu Bwana Musa ambaye alifungua
akaunti tatu za siri na pia kujenga hoteli kisiri bila mkewe kufahamu,
kisa hicho mwishoni kinaonyesha Bwana Musa alifariki ghafla na hivyo
kuleta msuguano mkali sana katika familia yake kuhusu mgawanyo wa mali.
Huku akijibu maswali ya mirathi yaliyojitokeza katika kisa hicho Ally
anataja, miongoni mwa hasara nyingine, kwamba kwanza haki ya urithi
imepotea, pili usiri wa baba umekuwa kikwazo katika familia kupata haki
ya msingi lakini tatu kwamba huenda wakati Bwana Musa anafariki kulikuwa
na pesa nyingi katika akaunti yake benki ambazo zingeisaidia familia
yake ambayo kwa mujibu wa kisa hicho hivi sasa familia hiyo inakumbwa na
janga kali la umaskini.
Katika kuelezea umuhimu wa wosia; Ally
aliendelea kusema kwamba wosia huondoa utata inapotokea kifo na vilevile
wosia huondoa chuki na fitna baina ya ndugu na jamaa.
Mwanamke anaweza kuwa msimamizi wa mirathi
Naye Faudhia Yassin ambaye ni mratibu wa kampeni ya TUNAWEZA kutoka
WLAC aliwaeleza wanakijiji kwamba Mwanamke amekuwa akitengwa sana katika
ugawaji mali hivyo ni muhimu jamii kutambua kwamba hata wanawake
waliofiwa na waume zao wanaweza kuwa wasimamizi halali wa mirathi.
Faudhia alisema ikitokea baba amefariki, familia ichukue cheti cha kifo
na kukipeleka mahakamani kuomba mahakama imuidhinishe waliyempendekeza
kuwa msimamizi wa mirathi.
Ndoa halali ni ipi?
Kundi la
tatu liliwakilishwa na Mama Shujaa wa chakula Grace G.D. Mahumbuka
kutoka Kagera pamoja na vijana wa Maisha Plus ambao ni Bakari Khalid
kutoka Shinyanga na Said Kawawa kutoka nchini Uganda.
Kundi hili
liligundua kwamba mtoto wa kike hathaminiki kama ilivyo kwa mtoto wa
kiume, lakini elimu pia ya uelewa juu ya mambo ya haki ni duni. Sehemu
ya kisa hicho iliwataja watu wawili wa jinsia tofauti walioishi pamoja
kwa kipindi cha miaka 12 bila kuwa na ndoa hata ya kimila.
Aidha
kundi hili lilipendekeza sheria ya ndoa ya Tanzania iboreshwe na kwamba
ifahamike kuwa mtoto wa kike ana haki ya kurithi sehemu ya mali ya
wazazi wake sawa sawa na ilivyo kwa mtoto wa kiume.
Waliendelea
kwa kushauri kwamba inapotokea tatizo katika ngazi ya familia baina ya
mke na mme basi aliyetendewa ukatili ajaribu kusuruhisha katika ngazi ya
familia ikishindana basi aende katika ustawi wa jamii, baraza la kata,
ofisi za ushauri wa kisheria za mashirika ya kiserikali na yasiyo ya
kiserikali kama itashindikana kote huko basi mwisho achukue hatua za
kisheria za kimahakama.
Akifafanua kuhusu hoja hii, Mwanasheria
Juvenile Rwegasira kutoka WLAC alisema kwamba watu wawili wa jinsia
tofauti wakiishi pamoja kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo na jamii
ikafahamu kwamba hawa ni mme na mke, hiyo kisheria inaitwa dhana ya
ndoa.
Mwanasheria Rwegasira alisisitiza kwamba ni lazima iwe
miaka miwili mfululizo na sio ile ya kuja miezi miwili na kuondoka na
kuja tena na kuondoka.
Hata hivyo, Bw. Rwegasira alitoa angalizo
kwamba ndoa hii ni rahisi sana kukanushika hivyo akasisitiza umuhimu wa
kuhitaji tamko la Mahakama kuidhinisha dhana ya ndoa.
Akiendelea Bw. Rwegasira alisema kwamba ndoa hii ni ya kienyeji mno na
haina cheti hivyo ikitokea mmoja amefariki inaleta shida sana kwenye
ugawaji wa mali.
Pata msaada wa kisheria BURE
WLAC ni
kituo cha msaada wa kisheria kwa wanawake. Kwa wenye matatizo ya
Mirathi, Ndoa, Ardhi, Elimu, Ajira, Matunzo ya Watoto na Mengineyo
wapige simu BURE kwenda namba 0800780100
Jumanne, 29 Aprili 2014
HALMASHAURI NA WADAU WA JIJI LA MWANZA WAANZA MAANDALIZI YA SHEREHE ZA KUADHIMISHA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA JUNI 16.
Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya jiji la Mwanza Bi Eluminata Mwita akisikiliza jambo kwa makini toka kwa wajumbe (hawapo pichani). |
Halmashauri pamoja
na wadau toka mashirika na taasisi za kutetea na kulinda haki za watoto jijini
Mwanza wameanza rasmi vikao vya maandalizi ya kuadhimisha sherehe za siku ya
mtoto wa Afrika inayoadhimishwa kila Mwaka Juni 16.
Kikao hicho kilichofanyika
katika ukumbi wa Halmashauri wa Jiji la Mwanza chini ya Afisa Maendeleo ya Jamii
wa Halmashauri hiyo Bi. Eluminatha Mwita wajumbe walikubaliana kuadhimisha siku
hiyo katika Kata ya Buhongwa, kwa Wilaya ya Nyamagana.
Siku ya mtoto wa
Afrika huadhimishwa kimataifa kote duniani kwa lengo la kutambua thamani, utu,
na umuhimu wa mtoto duniani. Maadhimisho haya hufanywa kila juni 16 tangu ilipotangazwa
kuwa siku rasmi mwaka 1991 na jumuiya ya umoja wa Afrika.
Akizungumza wakati
wa kufungua kikao hicho Afisa Maendeleo Jamii wa Jiji la Mwanza Bi. Eluminatha
Mwita alisema kuwa kauli Mbiu ya mwaka huu ni “Kuondoa Mila Zenye Kuleta Madhara kwa Watoto ni Jukumu Letu Sote”
na kufafanua kuwa kauli hiyo inalenga kuwasisitiza wazazi na walezi kuacha mila
potofu zenye kuleta madhara kwa watoto.
Bi Eluminatha
alisema kuwa “Kauli mbiu hiyo ina lenga kuangalia mila zote kandamizi na potofu
zinazotokana na jamii husika katika malezi ya mtoto na kusababisha madhara
mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa watoto wa mitaani, kubakwa kwa watoto, kukosa
elimu, afya na malezi bora pamoja na vifo kwa watoto hawa”.
Kikao hicho cha
kwanza kiliweza kuchagua viongozi wa kamati hiyo ya maandalizi, mwenyekiti aliyechaguliwa
ni Godfrey Salum huku katibu ni Devis Mrope na katibu msaidizi akichaguliwa
Francisca Michael, baada ya kupata viongozi kamati nne ziliundwa na wajumbe,
Kamati ya Uratibu, Mipango na Fedha, Kamati ya Usafiri na Ulinzi, Kamati ya
Mapambo na Burudani pamoja na kamati ya Hotuba na Habari.
Imeandaliwa
na Afisa Habari wa Kamati ya Maandalizi
Maadhimisho
ya Siku ya Mtoto wa Afrika - Mwanza
Hassan
Mrope
0713441892
Jisajili kwenye:
Machapisho (Atom)